Wagombea wawili wa nafasi ya urais wa Zanzibar wamesema hawaamini kama Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM, imependekeza wagombea watano tu kuwa wanafaa kuteuliwa kuwania urais wa visiwa hivyo.
Wamesema ikiwa mapendekezo hayo yametolewa itakuwa ni kinyume cha utaratibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wagombea hao, Balozi Ali Karume na mfanyabiashara maarufu, Mohammed Raza, ni miongoni mwa wana-CCM 11 wanaoomba ridhaa ya chama hicho kugombea urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Waliyasema hayo kwa nyakati tofauti katika mdahalo wa wagombea wa urais wa Zanzibar kupitia CCM uliofanyika jana kisiwani hapa na kudhaminiwa kwa ushirikiano wa kampuni za Vox Media na ASAM-PR.
Balozi Karume alisema kama CCM-Zanzibar imependekeza majina matano yaliyochapishwa jana katika vyombo vya habari, itakuwa imekwenda kinyume cha utaratibu wake na kwamba suala la kuwekewa alama lilishafutwa.
“Siamini kama kuna wagombea wamependekezwa, inawezekana maneno ya magazeti na kama ni kweli, basi tulipaswa kuambiwa wamepatikana kwa utaratibu gani, kama wamepigiwa kura au wameteuliwa,” alisema Balozi Karume ambaye ni mdogo wake Rais Amani Karume wa Zanzibar aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM visiwani hapa iliyopitia majina ya wagombea hao juzi.
Hata hivyo, alisema anaamini majina ya wagombea wote yatakwenda Dodoma, kwa vile kikao cha Zanzibar kinawajibika katika kuwajadili wagombea, kabla ya Kamati Kuu kuchagua majina matatu ya kupeleka Halmshauri Kuu ya Taifa (Nec) kwa ajili ya kupitisha jina moja la mgombea urais wa Zanzibar.
CCM ilifuta utaratibu wa wagombea wa nafasi hiyo kupigiwa kura Zanzibar na kuwekewa alama, baada ya matatizo yaliyojitokeza katika mchakato wa mwaka 2000 na 2005.
Kwa upande wake, Raza alielezea kushangazwa na taarifa kwamba majina matano ya wagombea, yalipendekezwa katika kikao cha kamati hiyo, bila kuelezwa utaratibu uliotumika na kuwapata wagombea hao.
“Bado siamini kama kuna wagombea bora wamependekezwa, nipo tayari kupokea maamuzi yoyote yatakayotolewa na chama changu,” alisema Raza.
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhani Ferouz, alisema maamuzi yote yaliopendekezwa katika kikao hicho, yataendelea kubakia siri hadi yatakapowasilishwa katika kikao cha Kamati Kuu.
“Si kila tunachokiamua kielezwe katika vyombo vya habari, CCM ina taratibu zake za kuendesha vikao na mapendekezo yalitolewa na kikao yataendelea kubakia siri hadi yatakapowasilishwa katika kikao cha Kamati Kuu,” alisema.
Naibu Katibu huyo alisema hayo baada ya kutakiwa na Nipashe jana, kufafanua utaratibu uliotumika katika kuwapata wagombea hao watano.
Habari kutoka ndani ya CCM ziliwataja wagombea watano waliopendekezwa kuwa wanafaa kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar ni Waziri Kiongozi Mstaafu, Dk. Mohamed Gharibu Bilal, Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna, Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman.
Wagombea wengine kati ya hao 11 waliojitosa kwenye kinyang’anyiro mbali na Naibu Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mohammed Aboud, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo, Hamad Bakari Mshindo, Muhamad Yussuf Mshamba, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi, Omar Sheha Mussa.
Wakati huo huo, wagombea nafasi ya urais wa Zanzibar wawili tu, waliojitokeza katika mdahalo kati ya wagombea 11 wanaoomba kuteuliwa na CCM kuwania nafasi hiyo.
Mwenyekiti wa mdahalo huo, Ali Saleh, alisema wagombea wote walipewa mialiko mapema, lakini wagombea watatu tu ndio walitoa sababu za kutohudhuria, baada ya kutingwa na ratiba nyingine za kazi.
Aliwataja wagombea waliotoa sababu za kutohudhuria kuwa ni Suleiman, Mshindo na Nahodha ambaye anahudhuria vikao vya bajeti ya mwaka wa fedha 2010/2011
“Tunashukuru kuweka historia kwa kuwakutanisha wagombea wa nafasi nyeti kama hii, pamoja na kuwa wagombea wengine wameshindwa kuhudhuria na kuwanyima haki wananchi wa Zanzibar, ya kutaka kufahamu kwa nini wanaomba ridhaa ya kupewa Urais,” alisema.
Kwa upande mwingine, Balozi Karume alisema ikiwa atafanikiwa kuwa Rais, ataijenga misingi mizuri ya kisiasa na kiuchumi, kwa kuimarisha sekta ya elimu ili kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha kiwango cha ubora wa elimu.
Pia alisema hatasita kusaini adhabu ya kifo kwa kwa mtu yeyote iwapo taratibu za kisheria zitazingatiwa kwa mujibu wa sheria.
Balozi Karume alishangazwa na Zanzibar kutoruhusiwa kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), badala yake kuruhusiwa nchi za Ruwanda na Burundi kwa madai kuwa mataifa hayo, yalikuwa sehemu ya Tanganyika kabla ya mgawanyo wa mipaka wakati wa ukoloni.
“Rwanda na Burundi ni nchi zilizokuwa sehemu ya Tanganyika, inakuwaje ziruhusiwe kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Zanzibar inyimwe,” alihoji.
Naye Raza alisema utatuzi wa kero za Muungano ni sehemu ya vipaumbele vyake ikiwa atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar.
Kamati Kuu ya CCM inatarajiwa kuwajadili wagombea nafasi ya urais wa Zanzibar wiki hii, kabla ya kupendekeza majina matatu katika kikao cha Nec kitakachochagua mgombea urais wa Zanzibar Julai 9 mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE
Monday, July 5, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment